1 John 5

1Yeyote anayeamini kuwa Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na yeyote ampendaye yeye ambaye ametoka kwa Baba pia huwapenda watoto wake. 2Kwa hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu -- tunapompenda Mungu na kutekeleza amri zake. 3Hivi ndivyo tunavyompenda Mungu kwamba twazishika amri zake. Na amri zake ni nyepesi.

4Kwa kuwa kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Na huu ndio ushindi wa kuushinda ulimwengu, imani yetu. 5Ni nani aliyeushinda ulimwengu? Ni yule aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

6Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu- Yesu Kristo. Hakuja tu kwa maji bali kwa maji na damu. 7Kwa kuwa kuna watatu washuhudiao: 8Roho, maji na damu. Hawa watatu hukubaliana. (Zingatia: Maneno haya “Baba, Neno, na Roho Mtakatifu” hayaonekani katika nakala bora za kale).

9Kama tunaupokea ushuhuda wa wanadamu ushuhuda wa Mungu ni mkuu kuliko huo. Kwa kuwa ushuhuda wa Mungu ni huu- kwamba anao ushuhuda kuhusiana na Mwanawe. 10Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu ana ushuhuda ndani yake mwenyewe. Na yeyote asiye mwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini ushuhuda ambao Mungu ameuleta kuhusu Mwanawe.

11Na ushuhuda ndio huu -- kwamba Mungu alitupa uzima wa milele, na uzima huu umo ndani ya Mwanawe. 12Aliye naye Mwana ana uzima. Asiyekuwa naye Mwana wa Mungu hana uzima.

13Nimewaandikia haya mweze kujua kwamba mnao uzima wa milele -- ninyi mnaoamini katika jina la Mwana wa Mungu. 14Na huu ndio ujasiri tulionao mbele zake, kwamba kama tukiomba kitu chochote sawa sawa na mapenzi yake, hutusikia. 15Na kama tunajua kwamba hutusikia -- chochote tumwombacho tunajua kwamba tunacho hicho tulichomwomba.

16Kama mtu amwonaye ndugu yake anatenda dhambi isiyopelekea kifo, yampasa kuomba na Mungu atampa uzima. Ninasema kwa wale ambao dhambi yao ni ile isiyopelekea kifo -- Kuna dhambi ipelekeayo kifo -- sisemi kwamba anapaswa kuomba kwa ajilli ya dhambi hiyo. 17Uasi wote ni dhambi -- lakini kuna dhambi isiyopelekea kifo.

18Tunajua ya kuwa aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi. Bali aliyezaliwa na Mungu hutunzwa naye salama daima, na yule mwovu hawezi kumdhuru. 19Tunajua kuwa sisi ni wa Mungu na tunajua kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu.

20Lakini twajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupatia ujuzi, kwamba tunamjua yeye aliye kweli na kwamba tumo ndani yake yeye aliye kweli, hata katika Mwanawe Yesu Kristo. Ni Mungu wa kweli na uzima wa milele. 21Watoto wapenzi, jiepusheni na sanamu.

Copyright information for SwaULB